TAKUKURU na Mahakama mabingwa wapya wa baiskeli SHIMIWI
service image
07 Sep, 2025
TAKUKURU na Mahakama mabingwa wapya wa baiskeli SHIMIWI

Wakati michuano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa nchini (SHIMIWI) inafunguliwa kesho tarehe 07 Septemba, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dotto Biteko, wachezaji wa timu za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) na Mahakama leo wameibuka mabingwa wa mchezo wa mbio za baiskeli kwa wanawake na wanaume za kilometa 50 na 30 zilizoanzia eneo la Igoma karibu na Makaburi ya Mv Bukoba jijini Mwanza.

Kwa upande wa wanaume ambao walishindana kwenye mbio za Kilometa 50, ambazo zilianzia eneo hilo la Igoma na kugeuzia eneo la Nyanguge zikiwa ni Km 25 kwenda na kurudi walipoanzia, mchezaji Chacha Ikwabe wa TAKUKURU alimaliza mbio hizo za kilometa 50 kwa wanaume kwa kutumia muda wa saa 1:21.47.

Mshindi wa pili kwa wanaume ameshinda Bw. Salum Ndambwe wa Wizara ya Ujenzi aliyetumia muda wa saa 1:26.21 na mshindi wa tatu ni Bw. Hassan Ligoneko wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora aliyemaliza kwa muda wa saa 1:27.02. Bw. Ligoneko ndiye alikuwa bingwa mtetezi.

Kwa upande wa wanawake ambao nao walianzia eneo la Igoma Makaburi ya Mv Bukoba kwa mbio za kilometa 30, zikiwa ni Km. 15 kwenda na kugeuzia eneo la Isangijo na kurudi walipoanzia, ubingwa umechukuliwa na Bi. Mwajabu Bwire wa Mahakama aliyetumia muda wa saa 1:06.35; akifuatiwa na aliyekuwa bingwa mtetezi Bi. Alavuya Mtalemwa wa Wizara ya Mambo ya Ndani aliyetumia saa 1:07.44 na watatu ameshika Bi. Donasia Tesha wa Wizara ya Fedha aliyetumia saa 1:12.34.