SERIKALI YADHAMIRIA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MICHEZO NCHINI
service image
14 Feb, 2022

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa (Mb) amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuboresha miundombinu ya michezo nchini hasa katika viwanja ili kuweza kuandaa timu Bora za Taifa ambazo zitapeperusha vyema Bendera ya Taifa katika mashindano ya kimataifa.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo tarehe 14 Februari, 2022 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika moja ya kumbi za uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam, mara baada ya kufanya kikao na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kujadili mustakabali wa maendeleo ya mchezo wa Soka pamoja na sakata la waamuzi linaloendelea nchini.

“sisi kama Serikali tumeweka msimamo kwamba tumejipanga vyema kuhakikisha kuwa tunaboresha miundombinu ya viwanja vyetu ili tuweze kuandaa timu zetu za Taifa hapo mbele,mpango wetu kama Serikali ni uboreshaji wa Shule za michezo 56 ambazo zimeibuliwa na dhamira yetu ni katika kila mkoani kuhakikisha kuwa tunakuwa na shule ambazo zitasaidia kuibua vipaji na kuendeleza vipaji katika maeneo hayo, sambamba na hilo Serikali tunategemea kujenga vituo vitatu vya michezo katika mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine ambayo wizara itafanyia kazi,”amesema Mhe. Mchengerwa.

Aidha Mhe. Mchengerwa ameitaka kamati ya waamuzi wa mpira wa miguu nchini kijitafakari na kuchukua hatua zaidi dhidi ya waamuzi ambao wameshindwa kutafsiri sheria za mpira wa miguu au kuonyesha viashiria vya Rushwa, huku akiiagiza TFF kuendesha Semina kwa waamuzi kwa kushirikiana na wataalamu kutoka taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU).

“pengine TFF wanakazi kubwa ya kufanya pamoja na kwamba wameshawaondoa waamuzi 13, lakini mpaka Ligi inakwisha tunajiuliza kama wizara watakuwa wamewaondoa waamuzi wangapi?,hivyo ni vyema kamati ya waamuzi ijitafakari kwa hiyo tunaliachia hili kwa TFF kwa sababu wao ndio wenye mamlaka, lakini pia wizara inaitaka TFF kuendesha Semina kwa waamuzi kwa kushirikiana na TAKUKURU kwa wale waamuzi ambao wanakwenda kinyume na kuashiria vitendo vya rushwa,”alisema Mhe. Mchengerwa