SERIKALI YAENDELEZA MCHAKAMCHAKA KUFANIKIWA JUMUIYA YA MADOLA

Serikali imeendelea na harakati tofauti kuhakikisha maandalizi ya michezo na wanamichezo watakaoiwakilisha nchi katika mashindano ya Kimataifa ikiwemo ya Jumuiya ya Madola inayotarajiwa kuanza Julai hadi Agosti 2022 nchini Uingereza wanaandaliwa vyema na kurudi na ushindi.
Hayo yamethibishwa leo Februari 10, 2022 baada ya Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Michezo Bw. Addo Komba kutoka Wizara yenye dhamana ya Michezo, Maafisa kutoka Baraza la Michezo la Taifa kwa pamoja na Katibu Mkuu kutoka Shirikisho la Riadha Tanzania (AT) Adv. Jackson Ndaweka akifuatana na Kocha wa riadha Fransis John kwenda kukagua kambi ya riadha itakayoanza kutumika kuanzia Jumamosi ya tarehe 12 Februari, 2022
"Kambi hii ilimsaidia Simbu kuiwakilisha nchi vizuri 2016 na kuwa mshindi wa tano (5) katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika nchini Brazil," alisema Kocha Fransis wakati wa safari kuelekea katika kambi hiyo.
Awali Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Michezo Addo Komba akizungumza na Afisa Tawala wa Chuo cha Viwanda vya Misitu ambao ndiyo wenye taasisi yenye kambi hiyo Ashir Kilemile alimweleza kuwa, hatuna budi kushirikiana ili wachezaji wailetee sifa nchi.
"Penye uwezekano hatuna budi kushirikiana ili wanamichezo wetu wafanikiwe na kuiletea nchi sifa,"alisema Komba.
Kambi ya mchezo wa riadha itahusisha wanariadha 15, wanaume 9 na wanawake 6 watakaoandaliwa katika kambi za ndani ya nchi naza nje ya nchi.