SERIKALI YAJIPANGA USHIRIKI MICHEZO JUMUIYA YA MADOLA.

Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na viongozi wa michezo shiriki wameendelea na kikao chenye lengo la kuweka mikakati ya nchi kuwa na uwakilishi mzuri katika michezo ya Jumuiya ya Madola inayotarajiwa kuanza Julai hadi Agosti 2022 nchini Uingereza.
Kikao hicho ambacho ni mwendelezo wa vikao vya maandalizi kimefanyika leo Januari 28, 2022, jijini Dar es salaam na kuongozwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa BMT Neema Msitha. Washiriki wengine ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Michezo Addo Komba pamoja na viongozi wa michezo itakayoshiriki katika mashindano hayo ikiwa ni; ngumi za wazi, Kuogelea, Judo, Riadha na wanyanyua vitu vizito vya watu wenye ulemavu.
Aidha, Msitha katika kikao hicho amewataka viongozi wa michezo inayoshiriki katika mashindano hayo kufanya maandalizi mapema ikiwemo kuanza kwa mafunzo ya ndani (Off camp training) pamoja ya kambi za kimataifa kufuzu kushiriki mashindano hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Michezo, Wizarani, Addo Komba alieleza kuwa, michakato ya wataalamu wa kimataifa kutoka katika nchi zilizopendekezwa inaendelea na makocha wa baadhi ya michezo ukiwemo mchezo wa riadha watawasili wiki ijayo.
Naye Katibu wa TOC Filbert Bayi ameshauri uwepo wa michezo ya majaribio pamoja na ile ya mashindano ya kimataifa ya kufuzu.