SINGO ASISITIZA KAMBI ZA TIMU ZA TAIFA KUELEKEA JUMUIYA YA MADOLA KUANZA MAPEMA

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Yusuph Singo Omary, amewasisitiza viongozi wa vyama mbalimbali vya michezo ambayo itashiriki katika mashindano ya Jumuiya ya Madola mwezi Julai hadi Agosti 2022 jijini Birmingham nchini Uingereza, kuhakikisha timu hizo zinaanza kambi mapema ili wachezaji wapate maandalizi ya kutosha kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Singo ametoa msisitizo huo leo tarehe 11 Februari, 2022 alipokutana na kufanya kikao na viongozi wa vyama vya michezo ya kuogelea, Ngumi, Riadha, Judo pamoja na kunyanyua vitu vizito kwa watu wenye ulemavu,kikao kilichofanyika katika moja ya kumbi za uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
“maagizo kutoka kwa viongozi wetu ni kwamba hatuna muda tena wa kuendelea kusubiri, ni lazima timu zetu zianze kambi mapema ili kupata maandalizi ya muda mrefu katika michezo yote, kwani Serikali ya awamu ya sita ina kiu kikubwa sana kuona tunakwenda na kurudi na medali kutoka katika mashindano ya Jumuiya ya madola pamoja na mashindano mengine ya kimataifa,”alisema Singo.
Aidha Singo amesema pia wachezaji watakaoingia kambini lazima wawe na viwango vya juu na Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta makocha Bora wa kuzinoa timu hizo na kuziongezea ujuzi zaidi kuelekea katika mashindano ya kimataifa.
“tunashukuru kwanza kabisa timu yetu kutoka wizarani na BMT ipo Mkoani Arusha na Kilimanjaro kwa ajili ya kukagua kambi itakayokaa timu ya Taifa ya Riadha, hivyo basi Serikali inafanya kila jitihada kuweka mazingira mazuri kwa wachezaji wetu lakini pia kutafuta makocha Bora wa kuzinoa timu zetu pamoja na kuziongezea ujuzi zaidi kuelekea katika mashindano haya makubwa,”alisema Singo.