SOKA KUNOGESHA MAADHIMISHO YA UHURU
service image
12 Jul, 2021

Mkurugenzi wa Idara ya Michezo  Wizara yenye dhamana ya michezo Yusuph

TIMU ya Taifa Stars inatarajia kushuka dimbani dhidi ya timu ya taifa Uganda katika mchezo wa kirafiki kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru utakaochezwa Desemba 9 mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar Es Salaam.

Katika maadhimisho hayo zinatarajiwa kushuka dimbani Timu za Taifa za wanaume Taifa stars na Timu ya Taifa ya Uganda lakini pia Timu za wanawake ya Tanzania (Tanzanite) watakaoshuka dimbani na timu ya uganda.

Akizungumza na wanahabari leo Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Yusuph Singo alisema kuwa timu za Uganda zinatarajiwa kuwasili leo tarehe 07 Disemba, 2021.

Alisema kuwa timu za Tanzania (Taifa star na Tanzanite zimeingia kambini juzi kwa ajili ya michuano hiyo na zinaendelea na mazoezi na mechi hizo ikianziwa na wanawake zitashuka dimbani majira ya saa 11 huku wanaume wakitarajiwa kuanza saa 2:00 usiku siku hiyo ya tarehe 9 Disemba.

"Mpaka sasa maandalizi yamekamilika na wachezaji wapo vizuri kwa ajili ya mechi hiyo ya kirafiki ambayo lengo kubwa ni kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania inayofanyika kila mwaka"alisema.

Aliongeza kuwa upande wa viingilio ni Sh. 2000 mzunguko huku VIP A na VIP B ni Sh. 5,000 lengo la kuweka viingilio hivyo ni ili kila mwananchi aweze kushiriki na kufurahia maadhimisho hayo.

"Tumeweka viingilio rafiki ili kila mtanzania aweze kushiriki tufurahie maadhimisho kwa pamoja," alisema.

Wachezaji wa Taifa Stars ni Metacha Mnata (Polisi Tanzania), Haroun Mandanda (Mbeya City), Musa Mbisa (Coastal Union), Nathaniel Chilambo (Ruvu Shooting), Kelvin Kijiri (KMC), Hans Masoud (Coastal Union), Nickson Kibabage (KMC) na Oscar Masai (Geita Gold).

Wengine ni Abdulrazack Mohamed (KMC), Lusajo Mwaikenda (Azam), Abdulmajid Mangalo (Biashara United), Nashon Naftari (Geita Gold), Tariq Simba (Polisi Tanzania), Sospeter Bajana (Azam), Hassan Nassor (Dodoma Jiji) na Abdul Hamis Suleiman (Coastal Union.

Pia wapo Meshack Abraham (Kagera Sugar), Cleophace Mkandala (Dodoma Jiji), Denis Nkane (Biashara United), Rashid Juma (Ruvu Shooting), Vitalis Mayanga (Polisi Tanzania), Anuary Jabir (Dodoma Jiji).