SPIKA WA BUNGE AWATAKA BMT KUSIMAMIA UIBUAJI WA VIPAJI

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amewataka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kusimamia uibuaji na uendelezwaji wa vipaji vya wanamichezo pamoja kuendelea kuifufua michezo iliyopotea.
Hayo ameyasema leo wakati akifunga tamasha la kimataifa la michezo la wanawake (Tanzanite) la siku tatu ambalo limeshirikisha mashindano ya michezo mbalimbali.
Mhe. tulia aliendelea kwa kuwataka BMT kuongeza hamasha ya kuitangaza michezo ya wanawake ili iongeze kupendwa na kuwa na wadau wengi kama ilivyo kwa wanaume.
"Niwapongeza Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na BMT kwa kuandaa tamasha hili ambalo ni kuunga mkono juhudi za Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika michezo ya wanawake," alisema Dkt Tulia.
Tulia ametoa pongezi kwa Wizara na BMT kuandaa Tamasha hilo lililoshirikisha michezo mbalimbali ikiwamo mchezo wa rede ambao umepotea kabisa.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Hassan Abbasi, alisema tamasha hilo litaendelea na wanawake waendelee kuunga mkono.