Taifa Stars imejipanga kwa Mikakati Thabiti-Kocha Hemed
service image
28 Jul, 2025

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman Ali [Morroco] amesema kuwa, timu imekuwa na kambi ya maandalizi ya wiki nne ili kuimarisha mshikamano, nidhamu, na utayari wa wachezaji.

Kocha Hemed alisema hayo, wakati wa kikao na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam tarehe 20 Julai, 2025.

“Mechi za kirafiki zilizopangwa zitatumika kama "kipimo cha mwisho" cha kujipima nguvu, kubaini maeneo ya kuboresha, na kuhakikisha wachezaji wako katika hali bora ya kiufundi na kimwili kabla ya michuano”, alisema kocha Hemed.

Katika kikao hicho, aligusia changamoto za majeruhi ambazo wachezaji wengine wamekuwa wakikabiliana nazo, pamoja na baadhi ya wachezaji kujiunga na kambi kwa kuchelewa kutokana na majukumu ya vilabu vyao.

Hata hivyo, alionesha imani kwamba benchi la ufundi limeweka mikakati madhubuti ya kushughulikia changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kuwapa wachezaji mafunzo ya ziada ya kujenga stamina na kurekebisha mikakati ya kiufundi.

"Nidhamu ya wachezaji na mshikamano wa timu ndiyo silaha yetu kubwa. Tunawahitaji wachezaji ambao wako tayari kutoa yote kwa jezi ya Taifa Stars," alisema kocha Hemed.

Aidha, kocha alisema kuwa ameweka mkazo kwenye uchezaji wa pamoja, kuboresha mbinu za ulinzi na ushambuliaji na wachezaji kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanaleta heshima kwa taifa, akiongeza kuwa sapoti ya serikali na umma imewapa motisha wa ziada.