TFF ENDELEENI KUWEKEZA NGUVU ZAIDI KATIKA SOKA LA WANAWAKE .

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Pauline Gekul (Mb) amelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuendelea kuwekeza zaidi katika soka la wanawake ambao wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Mhe. Gekul ameyasema hayo leo tarehe 23 Februari, 2022 alipokutana na kufanya kikao na viongozi wa vyama vya michezo kwa wanawake, kikao kilichofanyika katika moja ya kumbi za uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam, ambapo pia amesisitiza Ligi kuu ya wanawake nchini kuangaliwa kwa jicho la tatu na kuondoa changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza.
“ndugu zangu wa TFF endeleeni kuwekeza nguvu zaidi katika timu yetu ya mpira wa miguu kwa wanawake kwani mara zote wamekuwa wakitutoa kimasomaso katika mashindano ya kimataifa,lakini pia hii ligi yetu ya wanawake iangalieni kwa jicho la tatu kwa kuondoa changamoto ndogo ndogo zinazoweza kuleta dosari katika mpira wetu wa miguu,”amesema Mhe. Pauline.
Aidha Mhe. Pauline ameiagiza BMT kuendelea kuwa karibu zaidi na Chama cha Mchezo wa Netiboli Tanzania (CHANETA), huku akitoa maagizo kwa viongozi wa Chama hicho kuhakikisha Chaguzi kuanzia ngazi za chini zinafanyika kupata safu bora ya uongozi utakaorejesha heshima ya Chama na Mchezo wa Netiboli katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
“BMT endeleeni kuwa karibu zaidi na Chama hiki, na nyinyi viongozi hakikisheni chaguzi zinafanyika kuanzia ngazi za chini, ili muweze kuwa na safu bora ya uongozi utakaorejesha heshima ya Chama na Mchezo wa Netiboli katika ngazi ya kitaifa na kimataifa,”alisema Mhe. Pauline.