UONGOZI MPYA WA UMOJA WA GOFU TANZANIA (TGU), UMETAKIWA KUSHIRIKISHA VILABU VYOTE KATIKA MCHAKATO WA MAREKEBISHO YA KATIBA

Uongozi mpya wa Umoja wa Gofu Tanzania (TGU), umetakiwa kushirikisha vilabu vyote katika mchakato wa marekebisho ya katiba ili kuwa na katiba nzuri shirikishi ambayo kila mwanachama ataridhika nayo kwa maendeleo ya mchezo wa Gofu.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Benson Chacha, ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa TGU uliofanyika leo tarehe 14 Oktoba, 2022 katika ukumbi wa wazi wa klabu ya Gymkhana Morogoro, ambapo amesema pia uongozi huo unatakiwa kuandaa mashindano mbalimbali ya ndani ili kuwezesha wachezaji wadogo kushiriki na kupata uzoefu wa kufanya vizuri kimataifa.
“uongozi mpya mnatakiwa kurekebisha katiba yenu kwa kushirikisha vilabu vyote katika mchakato huu ili kuwa na katiba nzuri shirikishi, ambayo kila mwanachama ataridhika nayo kwa maendeleo ya mchezo wa gofu Tanzania,”alisema Chacha.
Aidha Chacha ameusisitiza uongozi wa mpya wa TGU kuanzisha utaratibu wa kushirikiana na chama cha Gofu wanawake (TLGU) ili kuweza kuendeleza mchezo wa Gofu na kuwawezesha katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wake mwenyekiti mpya wa TGU Bw. Gilman Kasiga amesema katika uongozi wake ataunda bodi ya ushauri ambayo itakuwa na baadhi ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa umoja huo.