WAZIRI MCHENGERWA ATOA AGIZO KWA WASIMAMIZI WA MICHEZO

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amewataka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kufuatilia vyama vya michezo mbalimbali vilivyopo katika ngazi ya wilaya ili kuleta maendeleo nchini.
Kauli hiyo alitoa leo tarehe 20 Oktoba, 2022 katika kongamano la kimataifa la michezo la wanawake lijulikanalo kwa jina la 'Tanzanite International Women Sports Festival) lililofanyika katika Ukumbi wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Waziri alisema sababu ya kushindwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ni kutokana na baadhi ya maeneo kukosa sapoti.
"Tunafanya vibaya kutokana na baadhi ya maeneo vyama vimekufa, wito wangu kwa BMT ni kwenda kufuatilia vyama hivyo kwa ngazi ya wilaya zote nchini, "alisema.
Mchengerwa alisema msingi imara unaanzia chini, hivyo wajibu wa BMT ni kufuatilia vyama hivyo katika ngazi ya wilaya ili kutambua changamoto zao.
"Kuna baadhi ya vyama vya wilaya vimekufa hivyo BMT mnapaswa kufuatilia kila wilaya kufahamu ili kuondoa changamoto, "alisema.
Aidha, Mchengerwa alitoa rai kwa vijana wenye vipaji kujitokeza ili kuviendeleza na kutimiza ndoto zao.
"Sasa tumeanza kampeni ya kutafuta vipaji ya mtaa kwa mtaa mkoa unaofuata sasa ni Arusha, wito kwa vijana ambao wana vipaji kujitokeza ili kuendeleza na kutangaza taifa letu, " alisema.
Tamasha la mwaka huu limehusisha michezo ya kimataifa wakiwemo wariadha kutoka Kenya, mabondia kutoka Zambia na wananetiboli kutoka Uganda pamoja na michezo mingine ya ndani ikiwemo soka, karate, kikapu, wavu, mpira wa mikono, jadi, wanyanyua vitu vizito ambapo tamati yake ni tarehe 22 Oktoba.