WAZIRI MKUU MHE. KASSIM MAJALIWA LEO OKTOBA 12, 2022 AMEFUNGUA RASMI MAONESHO YA WIKI YA VIJANA KITAIFA

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Oktoba 12, 2022 amefungua rasmi maonesho ya wiki ya vijana kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya Gymkhana Mkoani Kagera.
Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini ziendelee kutekeleza agizo la Serikali la kutenga maeneo rafiki yatakayowawezesha vijana kushiriki shughuli za uzalishaji mali ili kuwaepusha na kero ya ya kutekeleza majukumu yao ikiwemo biashara kwenye maeneo hatarishi.
“Maeneo haya ni lazima yawe na sifa zinazoendana na shughuli zinazofanywa na vijana”.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako ashirikiane na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Angela Kairuki ili kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ipasavyo.
Mbali na agizo hilo, Mheshimiwa Majaliwa amewaasa vijana kutumia vizuri fursa zilizopo nchini katika kujiletea maendeleo na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, ambayo inayoikabili dunia kwa sasa.
“Tanzania tunayo ardhi ya kutosha na yenye rutuba, tuna bahari, tuna maziwa na mito mikubwa, tunayo madini na sisi wenyewe kwa idadi yetu ni soko tosha la bidhaa mbalimbali, tutumie vizuri fursa hii ya kuwa na rasilimali nyingi kujipatia kipato.”
Waziri Mkuu ameongeza kuwa fursa nyingine kwa vijana ni uhusiano mwema wa kidiplomasia na nchi zote duniani.
“Fursa hii ikitumiwa vizuri na kundi la vijana wataweza kunufaika na kusonga mbele kimaendeleo”.