BMT: MASHINDANO YA TAEKWONDO YASAIDIA KUIBUA VIPAJ...

BMT: MASHINDANO YA TAEKWONDO YASAIDIA KUIBUA VIPAJI

14 Sep, 2026
BMT: MASHINDANO YA TAEKWONDO YASAIDIA KUIBUA VIPAJI

 

Mashindano ya Taekwondo yana mchango mkubwa katika kuibua na kukuza vipaji vya Watanzania, kwa kuwa kila mchezaji anayepata fursa anaruhusiwa kushiriki na kuonyesha uwezo wake.

Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa juma na Afisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Petro Chelula, wakati wa Mashindano ya Kombe la Taekwondo la Ubalozi wa Korea yaliyofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Nkuruma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Chelula amewataka mabalozi wa nchi mbalimbali waliopo nchini kuandaa mashindano ya michezo inayochezwa katika nchi zao, akisema hatua hiyo itasaidia kukuza michezo na kutangaza utamaduni wa nchi zao kupitia michezo.

Kwa upande wake Rais wa  Shirikisho la Taekwondo Tanzania (TTF), Abdallah Ally amewataka Watanzania kushirikiana na vyama vya michezo katika kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto, hususani katika mchezo wa Taekwondo.

Amesema Taekwondo inasaidia kuwajenga vijana kisaikolojia na kuwawezesha kufanya vizuri katika masomo kupitia michezo, huku akisisitiza umuhimu wa kupata wadhamini zaidi ili kuwezesha upatikanaji wa vifaa na kuandaa mashindano mengi.

Mashindano hayo yaliyoshirikisha wachezaji zaidi ya 100, yamefanikiwa pia kupata washiriki kutoka nje ya Tanzania. Mashindano hayo hufanyika kila mwaka kwa ushirikiano kati ya TTF na Ubalozi wa Korea, kwa lengo la kuibua vipaji na kuendeleza mchezo wa Taekwondo nchini.