Timu za mpira wa mikono za Ngome kwa wanaume na wanawake zimetwaa ubingwa wa Mashindano ya Nyerere Cup yaliyohitimishwa Oktoba 13, 2026, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuenzi kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Katika mchezo wa fainali kwa wanaume, Ngome ilitwaa ubingwa baada ya kuifunga timu ya SOS kutoka Burundi kwa mabao 29–22. Kwa upande wa wanawake, Ngome ilijinyakulia ubingwa baada ya kujikusanyia pointi nyingi zaidi katika mfumo wa ligi.
Akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo, Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Nuru Cassian, aliwapongeza mabingwa na kuwataka wachezaji ambao hawakufanikiwa kutwaa ubingwa kuendelea kujituma na kushiriki mashindano mengine ili kuongeza uzoefu na kuimarisha uwezo wao.
Aidha, alisema mashindano hayo ni sehemu ya kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere katika kutumia michezo kuunganisha jamii, huku akiwapongeza waandaaji na washiriki, wakiwemo wageni kutoka Burundi, kwa kuendeleza umoja na mshikamano kupitia michezo.