Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Mpira wa Mikono kwa Wanawake ya Kanda ya Tano Afrika, yatakayofanyika kuanzia Novemba 4 hadi 8, 2026, katika Viwanja vya Filbert Bayi, Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Akizungumza kuhusu mashindano hayo, Afisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Mikono Tanzania (TAHA), Vedastus Gunga, amesema jumla ya nchi 11 zitashiriki, zikiwemo Burundi, Djibouti, Misri, Ethiopia, Rwanda, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Uganda na wenyeji Tanzania.
Gunga ameongeza kuwa timu ya taifa ya wanawake inatarajiwa kuingia kambini Oktoba 20, 2026, kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kujiandaa na mashindano hayo.