Tanzania imeonyesha ushindani katika Mashindano ya Darts yaliyofanyika jijini Nairobi, Kenya, Septemba 18–20, 2026, yakishirikisha wachezaji kutoka Tanzania, Kenya na Uganda.
Mashindano hayo yalihusisha vipengele mbalimbali, ikiwemo PDC World Champs Qualifier, ADC Qualifier, African Continental Tour (ACT4) Women’s Series 4 pamoja na Grand Prix Finals.
Tanzania iliwakilishwa na wachezaji 10, wakiwemo wanaume tisa na mwanamke mmoja, Redempta Fabian Mwebesa, ambaye alifikia hatua ya robo fainali katika kipengele cha single kwa wanawake.
Kwa upande wa wanaume, Ramadhan Nalinga, Samuel Riunge na Rashid Raiyn mwenye umri wa miaka 17 nao walifika hatua ya robo fainali katika kipengele cha single mchanganyiko kilichokuwa sehemu ya mchakato wa kupata wachezaji watakaofuzu kushiriki PDC World Darts Championship katika ukumbi wa Alexandra Palace, London, Uingereza.
Licha ya kufanya vizuri na kuonyesha ushindani, Tanzania haikufanikiwa kupata nafasi ya kufuzu katika vipengele vilivyokuwa vikilenga kupata wawakilishi wa kwenda kushiriki mashindano makubwa ya Darts nchini Uingereza.
Mbali na ushindani wa uwanjani, wachezaji wa Tanzania walitumia jukwaa hilo kutangaza utalii wa Tanzania, hususan Mlima Kilimanjaro, kupitia jezi walizovaa, sambamba na kupata uzoefu na fursa ya kutambulika katika mashindano ya kimataifa.
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) linawapongeza wachezaji hao kwa kuiwakilisha Tanzania na kuitangaza nchi kupitia michezo, huku likimpongeza Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kumruhusu na kumwezesha mtumishi wake, Ramadhan Nalinga, kuungana na wenzake kuiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo.
BMT pia linawahimiza waajiri na taasisi mbalimbali kuwawezesha watumishi wenye sifa kushiriki na kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya michezo ya kitaifa na kimataifa, kwa kuwa ushiriki huo huongeza uzoefu, hujenga vipaji na kuchangia kuitangaza Tanzania kupitia michezo.