member photo
Bi. Neema Yotham Msitha
Katibu Mtendaji BMT

Barua pepe: info@nationalsportscouncil.go.tz

Simu: +255 734 220164

Wasifu

Salamu za Katibu Mtendaji

Kwa niaba ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ninafurahi kuwakaribisha katika tovuti yetu rasmi.

Baraza la Michezo la Taifa limepewa dhamana ya kusimamia, kuendeleza, kuratibu na kudhibiti maendeleo ya michezo nchini kwa mujibu wa sheria, sera na mipango ya maendeleo ya kitaifa. Baraza hili ndicho chombo cha juu cha usimamizi wa michezo nchini ambacho hufanya kazi kwa karibu na vyama vya michezo, taasisi za Serikali, wadau binafsi na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha michezo inachangia kikamilifu katika umoja wa kitaifa, ajira, maendeleo ya vijana, afya na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Tovuti hii ni jukwaa muhimu la utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu majukumu ya Baraza, programu, kanuni, mikakati na shughuli mbalimbali zinazoendelea. Aidha, inaonesha dhamira yetu ya kuzingatia uwazi, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wadau wote wa sekta ya michezo.

Tunatambua michezo kama ni nyenzo muhimu katika kukuza vipaji, kujenga nidhamu, kuimarisha uzalendo na kuinua hadhi ya Tanzania kimataifa katika masuala ya michezo. Katika muktadha huo, Baraza linaendelea kujidhatiti katika kuunda mazingira wezeshi kwa wanamichezo na taasisi za michezo ili kufikia viwango vya juu vya ubora, sambamba na malengo ya maendeleo ya taifa na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Nawahimiza wadau wa michezo hususani watalaamu, wasimamizi wa michezo, wawekezaji, washirika na wananchi kwa ujumla kushirikiana kikamilifu na BMT kupitia jukwaa hili,  ili kuendeleza michezo nchini.

Asanteni kwa kutembelea tovuti yetu. Tunatarajia kushirikiana nanyi katika kujenga sekta ya michezo iliyo imara, yenye ushindani na endelevu kwa maendeleo ya Taifa.

 

Bi. Neema Msitha

Katibu Mtendaji
Baraza la Michezo la Taifa