BMT NA TFF ZAPEWA KONGOLE KURATIBU MKUTANO WA CAF NA KUWALETA VIGOGO WA SOKA BARANI AFRIKA NCHINI
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda (MB), amewapongeza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na ShirIkisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kufanikiwa kuratibu vyema mkutano wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) uliofanyika nchini tarehe 13 Februari, 2026 Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Makonda ameyasema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 na kuongeza kuwa mkutano huo uliwaleta pamoja vigogo wa soka barani Afrika ukiwa na lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kukuza vipaji, kuimarisha ushindani wa vilabu na timu za Taifa, pamoja na kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya mpira wa miguu.
“Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni kielelezo cha uwezo wa nchi yetu kuandaa mikutano mikubwa na umeongezea hadhi ya Tanzania katika ramani ya soka Afrika hususan wakati mataifa yakijiandaa na fainali za AFCON 2027”, amesisitza Mhe. Makonda.
Amesema, ujio wa viongozi hawa unaweka wazi kuwa Tanzania inazidi kuaminiwa kama kitovu cha maamuzi makubwa ya michezo barani Afrika.

