BMT YATOA PONGEZI KWA WAOGELEAJI

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lawapa kongole waogeleaji kwa kuendelea kutimiza adhima ya Serikali ya kurudi na ushindi katika mashindano ya Kimataifa.
Kongole hizo zimetolewa usiku wa tarehe 19 Aprili, 2022 na mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa BMT ambaye ni Afisa Michezo Halima Bushiri wakati walipofika kuwapokea waogeleaji walioiwakilisha nchi kwa ushindi wa kumi bora na kurudi na medali 13 za ngazi tofauti katika mashindano ya kanda ya nne (Zone 4) yaliyomazika tarehe 18 Aprili nchini Zambia.
"Kama wasimamizi wa michezo nchini hatuna budi kuwapa pongezi wazazi wa watoto wa mchezo huu ambao mmekuwa mkijitoa kwa hali na mali kuhakikisha watoto wanacheza pamoja na kuiwakilisha nchi katika michezo mbalimbali za kimataifa, ushindi huu umechagizwa na ushirikiano wenu, hongereni sana,"alisema Halima.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha mchezo wa kuogelea nchini (TSA) Imani Alimanya amesema kuwa pamoja na hali ya baridi iliyokuwepo Zambia wachezaji walifuata maelekezo ya walimu wao na kujituma ndio maana wameibuka na ushindi huu.
"Ni mara ya kwanza tunashiriki katika mashindano haya ya kanda ya nne lakini wachezaji wameonesha uwezo hadi tumeibuka washindi wa 9 kati ya nchi 14 zilizoshiriki na zenye uzoefu,"alisema Alimanya.
Kwa upande wake Nahodha wa timu hiyo Collin Saliboko ameeleza kuwa mashindano hayo yameendelea kuwapa uzoefu ambao utawasaidia kufanya vyema katika michezo ijayo ya kimataifa ikiwemo ya Jumuiya ya Madola mwezi Julai hadi Agosti Nchini Birmigham nchini Uingereza.