BMT YAZISHUKURU MAMLAKA ZA MKOA WA IRINGA KUTOA USHIRIKIANO WA MAFUNZO YA USAJILI KIDIGITALI
service image
17 May, 2023

Msajili wa vyama vya michezo kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Riziki Majala ameishukuru mamlaka ya Mkoa wa Iringa kutoa ushirikiano, mafunzo ya mfumo wa usajili wa kidijitali kutolewa kwa wadau wa michezo katika mkoa huo.

Shukurani hizo amezitoa leo Mei 17, 2023 baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo yaliyoshirikisha Maafisa michezo wa halmashauri za mkoa huo sambamba na baadhi ya viongozi wa vyama vya michezo mkoani Iringa.

"Maafisa mchezo wa wilaya ndiyo chachu ya kamati za michezo za mikoa, tekelezani wajibu wenu ili michezo istawi katika maeneo yenu, andaae vikao na viongozi wa vyama vya michezo ili mvihuishe, na vifanye shughuli za michezo kihalali," alisisitiza Msajili na kuongeza kwa kusema kuwa;

"Nimefarijika kuwa na viongozi wa vyama vya michezo katika mafunzo haya, naombeni mkawe mabalozi wa kuwafundisha wengine mabadiliko haya ya mfumo wa usajili,"

"Niwape mwongozo kuwa ligi mnazoendesha kwa kushirikisha timu ambazo hazijasajiliwa ni makosa kisheria na mwenye makosa ni mwaandaaji. Natoa wito mkawaelimishe ambao hawajapata mafunzo haya,"

Kwa upande wake Afisa Utamaduni wa Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Iringa Steven Sanga ameishukuru BMT kwa mafunzo hayo yaliyowaunganisha maafisa hao ambao watabadilishana mengi.

"Tufanye kazi, thamani yetu na umuhimu wetu utaonekana pale tutakapokuwa na matokeo chanya," alisema Sanga.

"Matokeo chanya ni pamoja na kukuza michezo na kuimarisha afya kupitia kazi zetu katika maeneo yetu ya kazi," Alisema.

Kwa niaba ya Maafisa michezo wa Mkoa Iringa Afisa michezo wa Mufindi Henry Kapela ameishukuru BMT kwa mafunzo hayo na kuahidi kuwa wataenda kutoa mafunzo hayo kwa vyama na kuhamasisha usajili kwa wingi.

Naye mwakilishi wa viongozi wa vyama vya michezo, Katibu wa chama cha mpira wa miguu wanawake Mkoa Mwanaheri Kalolo amewaomba Baraza kuendelea kutoa elimu hiyo ili viongozi wa michezo wawe na uelewa na kufanya usajili kwa mfumo huo mpya.