NGUMI YAIHESHIMISHA TANZANIA MASHINDANO YA AFRIKA ACCRA
service image
24 Mar, 2024

Kikosi cha Timu ya Taifa ya Ngumi ya Tanzania almaarufu kama *"Faru Weusi wa Ngorongoro"* wamefanikiwa kuiheshimisha Tanzania katika michezo ya 13 ya Afrika Accra 2023 inayofungwa rasmi usiku wa leo katika Jiji la Accra, Ghana.

Kikosi hicho kimefanikiwa kushinda medali 3 za shaba katika mashindano hayo kutoka kwa wachezaji Light Heavyweight Yusuf Changalawe (Nahodha), Lightweight Ezra Paulo Mwanjwango na Cruiserweight Musa Maregesi.
Wachezaji wote hao wanatokea katika Klabu ya Ngome inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)

Katika sherehe za utoaji wa medali kwa washindi katika mchezo wa ngumi iliyofanyika jana usiku katika ukumbi wa Bukom Arena, Raisi wa Shirikisho la Ngumi Tanzania na mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Shirikisho la Ngumi la Bara la Afrika (AFBC) alipata kuwa mgeni rasmi katika kuwavalisha washindi wa Uzani wa Ligh Heavyweight 80kg kwa Wanaume na Cruiserweight 86kg ambapo Changalawe na Maregesi walikuwa moja ya washindi katika uzani hizo.

Kikosi hicho cha Faru Weusi wa Ngorongoro pamoja na wachezaji wa michezo mingine walioiwakilisha Timu Tanzania katika michezo hiyo, wanatarajia kurejea Dar es salaam kesho saa 9.40 usiku kwa Shirika la Ndege la Ethiopia kupitia Addis Ababa.

Kikosi hicho kikirejea Tanzania kitaendelea na mazoezi kujiandaa kushiriki mashindano ya Mandela *"Mandela Cup"* yatakayofanyika Durban, Afrika ya Kusini kuanzia tarehe 15-23 April, 2024.