CHANGALAWE AMPIGA TENA MMISRI NA KUTINGA NUSU FAINALI MASHINDANO YA MANDELA
service image
19 Apr, 2024

Nahodha wa kikosi cha Faru Weusi wa Ngorongoro Yusuf Changalawe amefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kumchakaza mpinzani wake Abdelgawwad Orabi Salah kutoka Misri kwa points 5-0 usiku Aprili 18, 2024 Afrika ya Kusini.

Huo ni ushindi wa pili kwa Changalawe dhidi ya mpinzani wake huyo mkubwa katika bara la Afrika ambapo alilipiza kisasi kwa ushindi wa points 4-3 katika hatua ya 16 bora katika michezo iliyopita ya Afrika Accra 2023 mwezi March.

Mchezo wa kwanza kukutana kwa mafahari hao wawili wa Afrika katika uzani wa Light-heavyweight 80kg ni katika fainali ya kufuzu Olimpiki kwa Bara la Afrika 2023 katika mji wa Dakar, Senegal na Changalawe alipoteza fainali hiyo na kukosa nafasi ya kwanza kushiriki Olimpiki ya Paris 2024.

Mashindano haya mapya ya Mandela yatafikia tamati kwa michezo ya fainali siku ya Jumapili tarehe 21-04-2024.

Tanzania inawakilishwa na Mabondia watano (5), na mpaka sasa wamebakia 2 ambao ni Changalawe na Azizi Chala waliopo katika hatua ya nusu fainali.

Mabondia Ezra Paulo Mwanjwango na Abdallah Mfaume "Nachoka" walipoteza mapambano yao Aprili 17, 2024.