FIFA FOOTBALL FOR SCHOOL
service image
15 Apr, 2024

Msigwa azindua mafunzo ya FIFA kwa Shule.

Katibu Mkuu wa Wizara Utamaduni Sanaa, Gerson Msigwa amesema kuwa Serikali kushirikiana na Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), hawatalala na kukubali juhudi zinazoletwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulimwenguni (FIFA) katika kuleta maendeleo ya soka la vijana kuanzia ngazi ya chini.

Kauli hiyo ameitoa leo Machi 15, 2024 wakati akizindua mafunzo ya mpira wa miguu kwa ajili yakufundisha watoto kwenye shule iliyoandaliwa na TFF kwa kushirikiana na FIFA na Shirikisho la mpira Barani Afrika (CAF) kwa ajili ya mafunzo kwa walimu 46 kutoka shuleni za msingi kutoka wilaya 16 nchini.

Msigwa, amewataka walimu waliopata mafunzo hayo kuyazingatia na kwenda kuwapa ujuzi huo watoto katika shule.

Alisema programu hiyo imekuja kimkakati kwa sababu nchi imeenda kuwekeza katika michezo kuanzia chini.

“Kwa sasa hatutalala na kukubali hizi juhudi zipotee, zinazotokana na mahusiano mazuri baina ya TFF na FIFA pamoja na CAF, walimu waliofaidika na programu hii wakahakikishe wanawatengeneza vijana vizuri," alisisitiza


Aliongeza kuwa nchi itakuwa mwenyeji wa AFCON 2027, kunatakiwa kuwa na maandalizi makubwa ikiwemo kuandaa timu za Taifa na inaanzia shuleni, walimu wanatakiwa kutumia vizuri mifumo hii maalum kuwapika vijana wa kesho.

“Tulipotoka huko nyuma tulikuwa na vipaji lakini sasa wanatakiwa kutengenezwa na kujua waishi vipi kimichezo, na Serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika michezo na inafanya kwa vitendo.

"Tayari tumeanza kwenye miundombinu, uwanja wa Arusha na Dodoma, vilevile tumeanza mchakato wa kujenga vituo vya Sanaa na Michezo kwa mikoa yote ya Tanzania, hii kwa ajili ya kuendeleza juhudu za michezo nchini,” alisema Katibu Mkuu Msigwa.

Naye Rais wa TFF, Wallace Karia alisema programu hiyo muhimu ni kwa ajili ya watoto kuanzia miaka 6 hadi 14 na wameanza kwenye shule za msingi.

Naye Meneja kutoka FIFA Antonio Sanchez alisema program hiyo ni maalum kwa vijana ambayo yana faida kubwa kwa mtoto kujifunza vitu vingine zaidi ya soka.