MAFUNZO YA MCHEZO WA JUDO

RAIS wa Chama cha mchezo wa Judo Tanzania (JATA) Zaid Hamis amepata fursa kwenda nchini Hangari kuhudhuria mkutano Mkuu utakaofanyika kuanzia Juni 9-16 mwaka huu.
Ameyasema hayo leo Aprili 11, 2025 wakati alipokuwa anafunga kliniki ya mchezo wa judo kwa wachezaji wa timu ya Taifa iliyofanyika kwenye chuo cha Polisi Kurasini kuanzia Aprili 07, 2025 na kuhitimishwa leo Dar es Salaam.
"Nimepata fursa ya kwenda kuhudhuria mkutano Mkuu nchini Hangari mkutano ambao utanisaidia kuwatafutia nafasi wachezaji wetu kwenda kufanya mazoezi nje ya nchi, alisema Hamis.
Katika hatua nyingine aliushukuru Ubalozi wa nchini Ufaransa kwa kuwaletea Mkufunzi Nicolas Malet ambaye aliiendesha Kliniki hiyo.
"Tunashukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa kutuletea Mkufunzi ambaye amewafanya wachezaji pamoja na makocha kufahamu sheria mpya za judo ambazo watakwenda kuwafundisha ambao hawajafanikiwa kuhudhuria Kliniki hii," alisema
Alisema mafunzo hayo yameshirikisha washiriki 68 kutoka klabu mbali mbali hapa nchini na kuahidi kuendelea kushirikiana na Ubalozi huo ili kuhakikisha kliniki kama hiyo inafanyika mara kwa mara.
Kwa upande wake Mkufunzi wa kliniki hiyo Nicolas Malet aliwashauri washiriki kwenda kuyafanyia kazi yale aliyowafundisha kwa lengo la kuviinua vipaji vyao.
"Kwa upande wa Tanzania wapo vizuri naamini yote niliyowafundisha yatakwenda kuwasaidia vile vile ninaushukuru Uongozi wa Chama cha Judo kwa ushirikiano mzuri walionionyesha tangu nilipofika mpaka leo tunamaliza,"alisema.