KARATE WAPATA WAKUWANOA
service image
30 Sep, 2022

Wakufunzi wawili wa kimataifa kutoka nchini Japan wamewasili nchini leo Septemba 30, 2022 kwa ajili ya kuendesha Mafunzo ya mchezo wa karate yatakayoanza Oktoba 4 hadi 8 Jijini Dar es Salaam

Akizungumza leo Septemba 30 mwaka huu katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam Mkufunzi mkuu wa Shirikisho la mchezo karate Tanzania kwa tawi la Japan (JKA/WF-TANZANIA), Sensei Jerome Mhagama amewataja wakufunzi hao kuwa, ni Shihan Naka na Shihan Okuma.

Mhagama ameeleza kuwa, wakufunzi hao wamewasili nchini Tanzania kwa ajili ya kambi ya siku saba ya mafunzo na mashindano ya mchezo huo yaani (GASHUKU) .

"Leo hii tumepokea ugeni kutoka nchini Japan ambao ni wakufunzi wetu wa mafunzo yatakayoanza wiki ijayo yatakayoenda sanjari na maadhimisho ya miaka 15 ya (JKA/WF-TANZANIA)," amesema Mhagama.

Zaidi ya mataifa 35 yatashiriki katika mafunzo na semina likiwemo taifa la Ujerumani, China pamoja na mataifa ya Bara la Afrika.