KIKAO CHA SERIKALI NA WADAU WA MPIRA WA MIGUU NCHINI.
service image
20 Mar, 2024

Watanzania watakiwa kuacha ushabiki na kuonesha uzalendo

Watanzania wametakiwa kuweka uzalendo na utaifa mbele kwa kuziunga mkono na kutoa hamasa kwa timu za Yanga na Simba katika michuano yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Rai hiyo imetolewa leo Machi 20, 2024 na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa kikao Cha Serikali na Viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi kuu (TPLB), sanjari na Viongozi wa klabu hizo Simba na Yanga kuweka mikakati ya ushindi.

Klabu ya Simba inatarajiwa kushuka dimbani dhidi ya Al ahaly ya Misri katika mchezo utakaopigwa Machi 29 mwaka huu, wakati klabu ya Yanga itashuka dimbani dhidi ya Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini katika mchezo utafanyika Machi 30, 2024 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Alisema kuwa, watanzania wanatakiwa kufanya mambo mawili ambayo ni kutoa hamasa kujaza uwanja na kuweka uzalendo katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya Ligi hiyo.

"Tumefanya kikao kati ya serikali, TFF, Bodi ya Ligi na viongozi wa timu ya Yanga na Simba, tumewasisitiza kuweka uzalendo na utaifa kwanza kwani wanawakilisha nchi ya Tanzania, tunaomba kushirikiana na Serikali ili kupata mafanikio, zitasema ifanye nini ili zifanye vizuri, sisi Kwa upande wetu tumeweka mambo sawa ikiwamo Uwanja na usalama "alisema Dkt. Ndumbaro.

Aliongeza kuwa" Rais wetu yupo tayari kusaidia michezo kimataifa na ameongeza dau la goli kutoka milioni tano na sasa milioni 10 ili timu zetu zifanye vizuri, kwani Serikali inatamani zifike fainali, ili ndoto hizi zitimie watanzania wanatakiwa kuunga mkono,"alisema.

Aliwataka viongozi wa vilabu hivyo kwenda kuzungumza na wasemaji wa timu hizo kutokubeza michezo hiyo.

Naye Rais wa TFF, Wallace Karia alisema, timu za Yanga na Simba wakiingia nusu fainali wataongeza pointi kwa Tanzania na klabu zao zitakazowezesha kwa idadi ya ushiriki wa timu nne katika msimu unaokuja katika michuano hiyo.

"Maelekezo mliyotupa tumeyapokea tutashirikiana na klabu hizi ili tufike nusu fainali na lazima tuingie tuna imani, uwezo wa kuingia nusu fainali," alisema.