HAFLA YA UZINDUZI WA MASHINDANO YA 'SAFARI LAGER CUP'
service image
08 May, 2025

Afisa Michezo mwandamizi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzo, amewapongeza Safari Lager kwa kushirikiana na Klabu ya Yanga katika kufanikisha mashindano ya kuibua vipaji kwa mara ya pili mfululizo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mashindano hayo, Maguzo alisema kuwa maendeleo ya michezo katika taifa lolote yanategemea uwekezaji wa rasilimali watu na fedha. Alisisitiza kuwa ni muhimu kuibua vipaji vipya ili kuendeleza michezo ya taifa kwa ujumla.

"Safari Lager wameamua kuungana na juhudi za serikali katika kuendeleza michezo, jambo ambalo tunalipongeza sana. Kupitia mashindano haya, vijana wengi wataweza kuonyesha uwezo wao na kupata nafasi ya kukuza vipaji vyao," alisema Maguzo.

Aidha, alieleza kuwa Baraza la Michezo la Taifa halina wasiwasi juu ya safari hii ya kuibua vipaji, na kuahidi kushirikiana kwa karibu na Safari Lager pamoja na Klabu ya Yanga kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa kwa kiwango cha juu.