HAFLA YA UZINDUZI WA MASHINDANO YA 'SAFARI LAGER CUP'
service image
08 May, 2025

Mkuu wa wilaya Kinondoni, Saad Mtambule, ametoa wito kwa vijana kote nchini kutumia mashindano ya Safari Lager 2025 kama jukwaa la kuonyesha vipaji vyao na kujitangaza kwa timu kubwa za soka hapa nchini.
 
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa msimu wa pili wa mashindano hayo, yanatarajiwa Julai 26 kwa mechi ya kirafiki kati ya timu ya vijana wa Safari Lager na klabu ya Yanga, Mtambule amesema mashindano hayo ni fursa ya kipekee kwa vijana chipukizi.
 
 "Tunatarajia kuona mashindano haya yakiwa bora zaidi katika awamu hii ya pili. Ni jukwaa ambalo vijana wanapaswa kulitumia kwa nguvu zao zote ili kuibua na kukuza vipaji vyao," amesema Mtambule.
 
Amesema kuwa maendeleo ya michezo nchini yanategemea uwekezaji mkubwa kuanzia ngazi za chini kama mitaani na vijijini.
 
"Tanzania hatuwezi kupiga hatua kubwa kwenye michezo kama hatutawekeza kuanzia ngazi za chini. Tunahitaji miundombinu ya kutosha, fedha na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, jamii na wadau wa michezo," ameongeza.
 
Mtambule pia alieleza kuwa licha ya changamoto ya uhaba wa viwanja jijini Dar es Salaam, kuwepo kwa mashindano kama haya kunasaidia kupunguza pengo hilo.
 
 
"Kama tungekuwa na vituo maalum vya kukuza soka kwa vijana, tungesaidia sana kutatua tatizo hili. Tunaamini mashindano haya yatatupa nafasi hiyo, na Serikali ipo tayari kushirikiana na wadhamini kuhakikisha mashindano yanakuwa salama na yenye mafanikio," amesema.
 
Mtambule ameeleza kuwa michezo ni chanzo cha ajira na maendeleo ya kiuchumi, na kwamba wilaya yake itaendelea kushirikiana na waandaaji pamoja na klabu ya Yanga kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata nafasi ya kung'ara katika soka.