MAANDALIZI YA UZINDUZI WA AFRICAN FOOTBALL LEAGUE YAANZA RASMI
service image
08 Aug, 2023

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amepokea ugeni wa timu ya wataalam wa African Football League chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ili kuanza maandalizi ya ufunguzi rasmi wa mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Oktoba 20, 2023 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya ziara ya ukaguzi wa maeneo ambayo yatafanyiwa ukarabati ili kuendana miongozo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) Agosti 7, 2023 jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema mazungumzo yao yalijikita zaidi kuangalia ubora wa Uwanja na maeneo ambayo yatafanyiwa ukarabati.

“Mazungumzo yetu yalijikita zaidi pamoja na ziara ya uwanja kuangalia ubora wa uwanja na maeneo ambayo tunaenda kuyafanyia ukarabati na mahitaji yao kwa ajili ya mechi ya ufunguzi ambayo kwa bara zima la Afrika itafanyika hapa katika uwanja huu wa Benjamin Mkapa” amesema Katibu Mkuu Bw. Yakubu.

Mashindano ya African Football League yanatarajiwa kuwa na manufaa mengi kiuchumi hapa nchini kwa kuwaleta wageni mashuhuri takriban 400 ambao watashiriki wakiwemo viongozi wa juu wa CAF na FIFA.

Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema wizara hiyo tayari imeshaingia mkataba na mkandarasi mkandarasi wa ukarabati huo Beijing Construction Engineering Group Co., Ltd. (BCEG) na kusisitiza kuwa mkandarasi huyo amekabidhiwa rasmi uwanja ili aendelee na majukumu yake ya ukarabati.