MAJALIWA ATOA AGIZO KWA TAMISEMI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Mhe. Kassim Majaliwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili kuwawezesha Maafisa Utamaduni na Michezo kutimiza majukumu yao ipasavyo.
“Ni Muhimu sasa TAMISEMI kuhakikisha mnatambua umuhimu wa kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo katika Halmashauri na mtambue kuwa ni moja kati ya vitengo muhimu ndani ya Halmashauri zenu na pia wapeni nafasi ya kutumia taaluma yao kutekeleza majukumu ndani ya Halmashauri ili tuone mafanikio ya sekta hizi”.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 5, 2022) wakati akifungua kikao kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo wa Mikoa na Halmashauri za Tanzania Bara kinachofanyika kwa siku (3) kuanzia tarehe 4-6 Aprili katika Ukumbi wa St. Gasper Jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini imekuwa kwa kiasi kikubwa na imeanza kuleta tija kwa maisha ya Watanzania kutokana na miongozo thabiti inayotolewa na Serikali.
“kwenye michezo tumeona namna ambavyo leo hii Tanzania inavyopata heshima kwa kuwa na timu za michezo mbalimbali zikifanya vizuri ndani na nje ya nchi, kwenye Sanaa tumeona namna ambavyo nchi hii imeweza kutangazwa vizuri na wasanii wengi kutoka ndani ya nchi, haya yote ni matokeo ya uratibu unaofanywa na Wizara, nawapongeza sana viongozi wa Wizara,"alisema.
Amesema Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeonesha kuwa na uwezo wa kutoa ajira kwa vijana wengi na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla huku akisema kwa sasa kwenye michezo kuna vijana wa Kitanzania wanaocheza michezo ya kulipwa katika nchi mbalimbali.
“Tuna wachezaji wetu wa mpira wa miguu kwa wenye ulemavu, sasa wanne wako nchini Uturuki kwenye vilabu vya kulipwa,"alisema.
Aidha Waziri Mkuu ameagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhakikisha inaandaa vikao kazi hivyo mara kwa mara ili kuwawezesha kupata mafunzo, kujua changamoto wanazopitia katika kutekeleza majukumu yao pamoja na kupata muda wa kufanya tathmini ya maazimio yanayotolewa katika vikao kazi hivyo.