MHE. BASHUNGWA AKONGA NYOYO ZA WANATASNIA YA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO
service image
06 Apr, 2022

Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Innocent ametoa agizo kwa watendaji wote wanaohusika na utekelezaji wa mabadiliko ya muundo wa kada za Maafisa Michezo na Utamaduni ulioidhinishwa unatekelezwa mapema iwezekanavyo ifikapo Julai 01, 2022.

Waziri Bashungwa amesema hayo Aprili 06, 2022 wakati akifunga kikao kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo ambapo alihimiza maandalizi ya utekelezaji wa muundo huo mpya yaanze mapema ili waweze kutoa huduma kwa Watanzania, kikao kazi kilichofanyika Jijini Dodoma.

Waziri Bashungwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia kuanzishwa kwa kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo na kumuagiza Katibu Mkuu Ofisi TAMISEMI kusimamia utekelezaji wa kuanzishwa Kitengo hicho cha Utamaduni, Sanaa na michezo kwa kuwa ni muhimu kama vitengo vingine nchini na lengo lake ni kuwahudumia Watanzania katika sekta hizo.

“Niwahakikishie, maelekezo ya Waziri Mkuu aliyayatoa hapa wakati wa kufungua kikao kazi hiki tutayatelekeza pamoja na Maazimio yanayohusu utekelezaji kwa upande wa TAMISEMI naahidi yatafanyiwa kazi na kutolewa taarifa kila baada ya miezi minne kama ilivyo kwa taasisi nyingine ili tunapokutana katika kikao kazi kingine, tuwe na taarifa ya jumla ya utekelezaji na tusonge mbele zaidi” amesema Waziri Bashungwa.

Katika kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Bashungwa amewaagiza Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kukaa mara moja na kuchambua maelekezo ya Waziri Mkuu ili yafanyiwe kazi kwa wakati kwa manufaa ya kuwahudumia Watanzania nchi nzima.

Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Wizara yake inashirikiana kwa karibu sana na TAMISEMI katika kutekeleza majukumu na maelekezo ya viongozi ili kufikia azma ya Serikali.

"Tunaenda kufanya mapinduzi makubwa ya kiutendaji katika Wizara hii, kila mmoja wetu aende kuchapa kazi,"alisisitiza Mhe. Mchengerwa.