MHESHIMIWA KIKWETE AWAPONGEZA SAMAKIBA
service image
20 Jun, 2023

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dokta Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza mchezaji Mbwana Ali Samatta pamoja na Msanii Ali Kiba kwa kubuni na kuanzisha Taasisi ya SAMAKIBA ambayo imekuwa ikikutanisha wadau mbalimbali kuandaa tamasha na kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia watu wenye mahitaji maalum nchini.

Mhe. Kikwete ametoa pongezi hizo leo tarehe 20 Juni, 2023 baada yakushuhudia mchezo wa Hisani uliondaliwa na taasisi ya SAMAKIBA katika uwanja wa Azam Complex Chamazi Jijini Dar es Salaam, ambapo timu ya mchezaji Samatta iliyosheheni nyota wa Ligi Kuu Tanzania Bara imefanikiwa kuibuka na ushindi wa magoli 4-2 dhidi ya timu ya mchezaji Ali Kiba.

"Niwapongeze sana wachezaji hawa kwa kubuni na kuanzisha taasisi hii ya SAMAKIBA, hakika ni jambo jema sana kwani limetukutanisha pamoja na tumefurahi kwa kweli umechezwa mchezo mzuri na wa kasi, ni Taasisi ambayo imekuwa ikitoa kwa jamii na leo hii inachangia vifaa tiba vya zaidi ya shilingi milioni mia moja na tisini (190, 000, 000) kwa watoto ambao wamezaliwa kabla ya wakati wao kufika, hongereni sana," amesema Mhe.Kikwete.

Mhe. Kikwete alihudhuria tukio hilo muhimu akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mheshimiwa Mwanahamisi Munkunda pamoja na Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha.