MSIGWA : KUSOGEZWA CHAN NI FAIDA KWETU
service image
15 Jan, 2025

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema kusogezwa mbele kwa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) 2024, inatoa muda wa kuendelea na maboresho makubwa zaidi ya miundombinu ya michezo.

Kauli hiyo amesema leo Jumatano ya Januari 15, 2025 kwenye hafla ya Kongamanano la wadau wa Michezo kuelekea michuano CHAN 2024 na fainali za AFCON 2027.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Jumanne , Januari 14, 2025, limetangaza kuahirishwa kwa michuano ya CHAN ambayo ilitakiwa kufanyika Februari 1 hadi 28 lakini sasa kusongezwa mbele hadi Agosti mwaka huu, Tanzania, Kenya na Uganda wakiwa wenyeji wa michuano hiyo.

Amesema Serikali imepokea taarifa hiyo kwa mikono miwili ya kusogezwa mbele kwa mashindano hayo ambayo yanawapa nafasi ya kuendelea kuboresha zaidi miundombinu kuwa bora zaidi na kuvutia.

“Tanzania tulishafanya maandalizi ya kutosha kwenye kiwanja cha Meja Jenerali Isamhuyo, Gymkhana na Uwanja wa Law School vilikuwa tayari kwa asilimia 90.

“Kusogezwa mbele kwa mashindano hayo tunapata nafasi ya kufanya vizuri katika ujenzi wa viwanja vya mazoezi na kuboresha zaidi katika maeneo ya kuchezea na kufanya kuvutia zaidi,” amesema