MSITHA AAHIDI KUITENDEA HAKI IMANI WALIONAYO KWAKE VIONGOZI
service image
01 Apr, 2022

Neema Msitha Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) amesema kuwa ataitendea haki imani walionayo kwake Viongozi wa Wizara waliokaa na kuona anafaa na Waziri kumthibitisha katika nafasi aliyokaimu tangu mwaka 2019.

"Na mimi nitahakikisha imani waliyonayo kwangu naitendea haki kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo vikiwemo vyama vya michezo Wizara, taasisi binafsi na makampuni mbalimbali,"alisisitiza Msitha.

Msitha ameyasema hayo alipoulizwa na Mwandishi wa habari kuwa, anawaambia nini Watanzania na wadau wa michezo baada ya kuthibitishwa kuwa Katibu Mtendaji wa BMT, uthibitisho uliotolewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa kongamano la wadau wa michezo la kueleza mafanikio ya sekta hiyo ndani ya mwaka mmoja wa Utawala wa awamu ya Sita (6) chini Rais Samia Suluhu.

Msitha ameeleza kuwa jamii ielewe kuwa tofauti ya mwanamke na mwanamme ni jinsia tu na kusema kuwa katika majukumu hakuna utofauti na pengine mwanamke anaweza kufanya majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Aidha, ameeleza kuwa ataendelea kuhamasisha wanawake katika ngazi za uongozi wa vyama vya michezo ili wawahamasishe na wengine.

"Jamii iondoe dhana potofu kuwa mwanamke hana uwezo, ni imani yangu kwamba ukimpa nafasi mwanamke anaitendea haki, na mimi ahadi yangu ni kwamba kwakuwa wanawake tuko wengi natamani kuwapa nafasi wanawake ili wawashike wengi,"

Aliendelea kwa kusema kuwa, ataendelea kushirikiana na vyama vya michezo yote na kuhakikisha kuwa penye kuhitaji kusaidia BMT itasaidia kulingana na uwezo ili michezo iiwakilishe vyema nchi katika mashindano mbalimbali ya ndani na nje.

Aidha, Msitha alipoulizwa kuhusu kupotea kwa michezo ya Jadi, alieleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha michezo yetu ya jadi inarudi na kusema kuwa kwasasa katika matukio mengi ya kitaifa lazima yahusishe michezo ya jadi ili wananchi na vivazi vya sasa viielewe michezo hiyo

"Tunao viongozi wa michezo ya jadi kwa sasa ambao wapo vizuri na wanaendelea kuitangaza, kila nchi ina nembo yake na sisi tutaisimama na ipo siku itachezwa duniani kama kabbadi, judo,"alisisitiza.