MSITHA ATAJA MATUMIZI YA RASILIMALI ZA MFUKO WA MAENDELEO YA MICHEZO
service image
05 Apr, 2022

MSITHA ATAJA MATUMIZI YA RASILIMALI ZA MFUKO WA MAENDELEO YA MICHEZO

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bi. Neema Msitha ameeleza kuwa, matumizi ya rasilimali za mfuko wa maendeleo ya michezo yatafuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya matumizi ya fedha ya Serikali kama inavyotolewa kila mwaka wa fedha wa Serikali.

Amezungumza hayo leo tarehe 05 Aprili, 2022 wakati akiwasilisha mada kuhusu kuundwa kwa mfuko wa maendeleo ya michezo ambao unatokana na michezo ya kubashiri na unaosimamiwa na BMT.

"Mfuko huu upo kwa ajili ya maendeleo ya michezo lakini matumizi yake lazima yaende kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na miongozo ya matumizi ya fedha za serikali kama inavyotolewa kila mwaka wa fedha,"alisema Msitha.

Aidha, Katibu Mtendaji wa BMT ameeleza majukumu ya mfuko huo kuwa ni kuwezesha kukuza maendeleo ya michezo kwa kutafuta na kupokea fedha kutoka vyanzo mbalimbali kugharamia shughuli za michezo.

Kugharamia timu za Taifa na wanamichezo wanaoiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa, Kugharamia, Kugharamia ujenzi, ujenzi ukarabati, matengenezo ya miundombinu ya michezo na ununuzi wa vifaa na zana za michezo.

Kuwezesha na kugharamia mafunzo kwa wanamichezo, kuwezesha Wizara yenye dhamana ya michezo kutekeleza majukumu yanayohusiana na maendeleo ya michezo, kugharamia utekelezaji wa shughuli za michezo kwa maelekezo ya Baraza na kuwezesha sekta ya michezo kukua na kutumika kama mlango wa ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mengine ni kukuza afya za watanzania, kuwezesha ukuaji wa masoko, ukuzaji wa vipaji, matangazo, harambee na matukio ya kitaifa na kimataifa ya michezo pamoja na kuwezesha dhana ya utawala bora katika michezo.

Lakini pia, Msitha ameainisha vipaumbele vya mfuko ikiwa ni pamoja na kusaidia timu za taifa, kusaidia ujenzi wa miundombinu ya michezo, vifaa vya michezo na kuwezesha mafunzo kwa wataalam wa michezo na wanamichezo.