MSITHA AVITAKA CHANETA NA CHANEZA KUBORESHA UHUSIANO

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Yotham Msitha, amewataka viongozi wa Chama cha mchezo wa Netiboli Tanzania (CHANETA) na Chama cha mchezo wa Netiboli Tanzania Visiwani (CHANEZA) kuwa na utashi wa mawasiliano ili kuendelea kuboresha uhusiano uliopo kwa maendeleo ya mchezo wa Netiboli nchini.
Msitha ametoa rai hiyo leo tarehe 28 Septemba, 2022 alipokutana na kufanya kikao na viongozi wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), CHANETA na CHANEZA katika moja ya kumbi za uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ambapo amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, imewekeza kwa kiasi kikubwa katika Tasnia ya michezo hivyo ni vyema viongozi wa vyama wakaendana na kasi iliyopo kuendelea kupiga hatua ili kufanya vizuri kitaifa na kimataifa.
“kitu kikubwa ninachokiona ambacho kimetufikisha hapa, ni kukosa utashi wa mawasiliano, hivyo ni vyema tukawa na utashi wa mawasiliano baina yetu ili tuendelee kuboresha kuboresha uhusiano uliopo kati ya Bara na Visiwani kwa maendeleo ya mchezo wa netiboli nchini,”alisema Msitha.
Aidha Msitha amewasisitiza viongozi hao kuandaa mikakati ya pamoja na ya muda mrefu katika maandalizi ya timu ya Taifa,ili kupata wachezaji bora watakaoleta ushindani katika mashindano ya Kimataifa.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BTMZ Said Kassim Marine amesema ni vyema viongozi wa CHANETA na CHANEZA wakaandaa andiko la makubaliano mapya yakayoonyesha namna watakavyoshirikiana na kuliwasilisha Serikalini kwa utekelezaji zaidi.