MSITHA: FANYENI JITIHADA ZA KUWAWAKILISHA VYEMA WATANZANIA
Na. Najaha Bakari - DSM
Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amewasihi waogeleaji kufanya jitihada za kuiwakilisha vema nchi katika mashindano ya Kanda ya nne, yanayotarajiwa kuanza Aprili14 hadi 18 Lusaka nchini Zambia.
Amezungumza hayo leo Aprili 11, 2022 kwa waandishi wa Habari wakati wa kukabidhi bendera na kuwataka waogeleaji hao wakafanye jitihada za kuhakikisha wanakwenda kuipeperusha vema bendera ya nchi katika mashindano hayo, tukio lililofanyika uwanja wa Benjamin Jijini Dar es salaam.
Msitha alisema kuwa Serikali itashirikiana na Chama na kuhakikisha mchezo huo unapiga hatua na baadaye kuleta medali katika mashindano mbalimbali kwa miaka ya baadaye.
"Mnakwenda kuuwakilisha umma wa mamilioni ya watanzania, fanyeni jitihada za kuhakikisha mnafanya vizuri na tunatarajia mlete medali ya michezo hiyo ya kanda ya nne,” alisema Neema.
Aliupongeza uongozi wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) kwa yale wanaoyofanya kutokana na mchezo kuimarika, hasa kwa vijana wadogo kwenda kushindana katika mashindano hayo.
Naye Mwenyekiti wa TSA, Imani Alimanya alisema waogeleaji 18, kuanzia umri wa miaka 11 na kuendelea wanatarajiwa kuondoka kesho tarehe 12 Aprili, 2022 kuelekea katika mashindano hayo.
Alisema Tanzania imepata mwaliko na watayatumia kupata uzoefu katika maandalizi ya mashindano ya Kimataifa ya Jumuiya ya Madola.
Kwa upande wake Nahodha wa timu hiyo Collins Saliboko ameahidi kuwa wanakwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo.