OBFT KUENDELEA NA MIKAKATI YA KUJIIMARISHA NA MICHEZO YA JUMUIYA YA MADOLA
service image
13 Apr, 2022

Shirikisho la Ngumi za Wazi Nchini (OBFT) linatarajiwa kufanya mashindano ya majaribio ya Kimataifa kuanzia tarehe 10-14 June, 2022 ili kujiweka kimafanikio katika michezo ya Jumuiya ya Madola inayotarajiwa kuanza Julai 28 hadi Agosti 08, 2022 Birmigham nchini Uingereza.

OBFT imeendelea na mikakati hiyo kufuatia maelekezo ya Serikali kuwa michezo yote inayoshiriki katika michezo hiyo lazima wajiandae kwa mashindano ya ndani naya kimataifa ili kuiwakilisha nchi kwa mafanikio katika michezo hiyo.

Mikakati hiyo ya OBFT imedhihirishwa leo Aprili 13, 2022 walipokaa na maafisa wa Baraza la Michezo la Taifa kupanga mipango tofauti ya kufanyika kwa mashindano hayo.

Kaimu Katibu wa OBFT Mohamed Abubakari katika maongezi yake wakati wa kikao hicho aliihakikishia serikali kuwa wanao wachezaji wazuri wanachohitaji ni mazoezi kutoka kwa mabondia wenye uzoefu.

"Wachezaji tunao wazuri wanachotaka ni mazoezi tu ya kutoka kwa mabondia wenye viwango na uzoefu,"alieleza Kaimu Katibu wa OBFT

Mashindano hayo yatahusisha nchi sita (6) ikiwemo Malawi, Zambia, Kenya, Uganda, Zimbabwe na mwenyeji Tanzania. Lakini pia Mabondia wa Tanzania watashiriki mashindano mengine ya majaribio nchini Uganda tarehe 18-21 Mei, 2022 yatakayohusisha nchi nne Mwenyeji Uganda, Tanzania, South Sudan na Burundi.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa ya mtindo wa mzunguko/ligi ili kuwasaidia mabondia waweze kijipima na mabondia wa viwango tofauti tofauti na kuongeza uzoefu zaidi.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Maafisa wa BMT Halima Bushiri, Allen Alex kutoka Idara ya Michezo na Najaha Bakari Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na kutoka OBFT kilwakilishwa na Kaimu Katibu Mohamed Abubakar na wajumbe Mafuru Mafuru, Mohamed Rajabu, Zainabu Shamte na Donath Massawe.