WAZAZI WATAKIWA KUWAPA WATOTO WAO NAFASI YA KUSHIRIKI MICHEZO MBALIMBALI
Afisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Charles Maguzu amewaasa wazazi kutokuwa wabaguzi wa michezo ambayo wanataka watoto wao washiriki badala yake wawaruhusu watoto hao kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo mchezo wa Vishale (Darts).
Maguzu ameyasema hayo siku ya leo Novemba 09, 2023 wakati wa hafla ya kukabidhi bendera kwa kikosi cha timu ya Taifa ya Mchezo wa vishale ambacho kinatarajiwa leo kwenda jijini Mombasa nchini Kenya kwa ajili ya kushiriki kwenye mashindano ya Afrika Mashariki yanayoanza tarehe 10 hadi Novemba 12, 2023.
Maguzu alisema kuwa matarajio ya Serikali ni kwamba kikosi hicho kitarudi na ushindi na kueleza kwamba wana imani wachezaji waliopata fursa wamepatikana kihalali na watakwenda kufanya vizuri na kurudi na ushindi.
"Kwa niaba ya Serikali tuwapongeze viongozi kwa juhudi za kukuza mchezo huu na wadhamini waendelee kuwaamini na kuwashika mkono na kuwataka wakafanye vizuri katika mashindano hayo," alisema Maguzu .
Aidha, ametoa rai kwa viongozi wa mchezo huo kuhakikisha unaenea kwenye maeneo mbalimbali na kuchezwa katika ngazi ya shule Ili kupata wachezaji wengi watakaoshiriki Mashindano ya ndani na kimataifa.
Naye Nahodha wa timu yaTaifa ya Mchezo huo Johakim Mollel, àmesema wamejipanga kufanya vizuri katika mashindano hayo na kueleza kuwa, wanakwenda kupambana, kushindana na sio kushiriki katika mashindano hayo.
Msafara wa kikosi hicho unaundwa na watu nane wakiwemo wachezaji sita wanaume wakiwa wanne ambao ni Noah Issa, Johakim Mollel, Yohana Kisau na John Mlay huku wanawake wakiwa wawili Happynes Modah na Irene Kihupi sambamba na viongozi wawili.
Mashindano hayo yatahusisha nchi tano ikiwemo mwenyeji Kenya, Uganda Tanzania, Rwanda na Burundi.