SERENGETI GIRLS WAZAWADIWA MILIONI 40 BAADA YA KUFIKA ROBO FAINALI KOMBE LA DUNIA
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Mohamed Mchengerwa amekabidhi Hundi ya Shilingi Milioni 40 kwa Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya Miaka 17 (Serengeti Girls) baada ya kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia yanayoendelea nchini India.
Mhe. Mchengerwa amekabidhi Hundi hiyo ambayo aliahidi mwezi Septemba wakati anawaaga Serengeti Girls walipoenda Kambi nchini Uingereza na baadae kwenye mashindano.
"Hongereni sana vijana, mmepambana na mmelitangaza Taifa, nawasihi msibweteke endeleeni kufanya mazoezi ili muweze kuwa na afya njema na muweze kuwa na uwezo mzuri zaidi wa kucheza zaidi" amesema Mhe. mchengerwa.
Ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anawapongeza sana vijana hao na ameahidi kuendelea kuwawezesha vijana hao waendelee kukuza vipaji na kusaidia Taifa lao.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Damas Ndumbaro amewasisitiza vijana hao kuendelea kujituma zaidi ili waweze kupata nafasi katika Vilabu vikubwa Duniani na baadae kuunda timu Bora ya Taifa ya Wanawake.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul, ameishukuru Serikali pamoja na Shirikisho la mpira wa Miguu kwa kuiwezesha timu hiyo kushiriki na kufuzu hadi hatua hiyo ya robo fainali.
Serengeti Girls imefika hatua ya robo fainali ya Mashindano hayo baada ya kucheza mechi tatu dhidi ya Japan, Ufaransa pamoja na Canada ambao baada ya kutoa sare ya goli moja kwa waliwapa tiketi ya kwenda robo fainali ambayo walicheza na Colombia na kufungwa magoli 3 - 0.