SERENGETI WAPEWA MBINU ZA USHINDI KOMBE LA DUNIA
service image
21 Sep, 2022

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa amewaasa wachezaji wa timu ya mpira ya wanawake chini ya miaka 17 (Serengeti Girls) kuonyesha uzalendo, kufuata maelekezo ya mwalimu na kujituma ndo silaha ya kufanya vizuri katika mashindano ya kombe la Dunia kwa wasichana chini ya umri huo yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Oktoba mwaka huu nchini India.

Kauli ya Waziri huyo ameitoa leo Septemba 21 katika hafla ya kuiaaga timu hiyo ya Taifa ya wanawake chini ya U -17, Serengeti Girls ambao wanatarajia kuondoka Septemba 25, mwaka huu kuelekea nchini Uingereza kwa ajili ya kambi katika klabu ya Southampton kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo.

Akizungumza katika hafla hiyo Mchengerwa alisema wachezaji wakijituma, kupambana na kuweka bidii katika michezo hiyo ana matarajio makubwa ya timu hiyo kufanya vizuri na kucheza robo fainali, nusu na fainali ya kombe la Dunia.

"Tumejiridhisha kambi na klabu ya Southampton itakuwa sehemu nzuri kwa timu yetu kupata maandalizi mazuri pamoja na kucheza mechi kadhaa za kirafiki kabla ya kwenda nchini India katika mashindano hayo," alisema Mhe. Waziri.

"Hatuna sababu ya kushindwa, kama wachezaji wakiweka bidii, kuacha uvivu na kujitoa, ikiwezekana kuvunjika uwanjani kwa ajili ya kuletea heshima kwa Taifa, hii ndio Kiu ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan na watanzania," alisema Mhe. Mchengerwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Bima ya Taifa( NIC), Elirehema Doriye alisema umetoa bonasi kwa timu wakiingia hatua ya robo fainali watazawadiwa sh. Milioni 40, nusu fainali sh. Milioni 80 na fainali sh milioni 100.



Alisema wachezaji wanapaswa kujituma ili kuleta ushindani na ushindi nchini kwa ajili ya kuiletea heshima taifa.

"Jambo la muhimu ni kwenda kupambana sisi kama kampuni ya bima tupo na nyinyi mwanzo mwisho kuhakikisha mnakuwa salama katika suala nzima la bima ya afya," alisema.

Aidha, alisema jumla ya dola laki tano na elfu 81 zitatumika katika suala zima la masuala ya bima kwa wachezaji wa timu ya Taifa ya Soka kwa watu wenye Ulemavu 'Tembo warriors'.

Kwa upande wa Kocha wa Bakari Shime, alisema malengo ni ushindi.