SERIKALI YATOA MWELEKEO MPYA KUKUZA MCHEZO WA POOLTABLE NCHINI
service image
07 Jan, 2026

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha mchezo wa Pooltable unaendelea kupiga hatua nchini na kuwakilisha vyema Taifa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa Januari 6, 2025, wakati wa mazungumzo maalum kati ya Naibu Waziri huyo na viongozi wa Chama cha Pooltable Tanzania, yaliyolenga kujadili maendeleo, changamoto na fursa zilizopo katika mchezo huo. Mhe Mwinjnuma amekutana na viongozi hao akitimiza ahadi yake ya kukutana nao alipohudhuria na fainali ya mashindano ya wakali wa pooltable.

Mhe. Mwinjuma amesema kuwa Pooltable ni miongoni mwa michezo inayofanya vizuri katika mashindano ya Afrika, hali inayotoa taswira chanya kwa Tanzania na kuifanya Serikali kuona umuhimu wa kuendelea kuwekeza na kuupa msukumo zaidi mchezo huo.

Ameeleza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa michezo ili kuimarisha mifumo ya usimamizi, kuongeza ushindani na kufungua fursa zaidi kwa vijana wenye vipaji katika mchezo wa Pooltable.

Kwa upande wake, mlezi wa mchezo wa Pooltable nchini, Ndugu Mrisho Mpoto, ameishukuru Serikali kwa juhudi zake za kubadili mtazamo wa jamii kuhusu mchezo huo. Amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa dhana potofu iliyokuwepo kwamba Pooltable ni mchezo wa kihuni, na badala yake kuitambua kama mchezo halali unaotoa ajira, kipato na fursa za kimataifa kwa vijana wa Kitanzania.