SHIRIKIANENI NA VYAMA MNAVYOVISIMAMIA KUVIFUFUA NA KUENDESHA MASHINDANO
service image
13 Mar, 2022

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limeutaka uongozi wa Kamati ya Paralimpiki Tanzania (TPC) kuhakikisha wanashirikiana kwa karibu na vyama wanavyovisimamia kuendesha mashindano pamoja na kulipa ada zao ili kuendelea kuwa wanachama hai na kupata wachezaji watakaoleta ushindani katika mashindano ya kimataifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Riadha Taifa kwa watu wenye ulemavu yaliyoandaliwa na kamati ya Paralimpiki Tanzania (TPC) Afisa Michezo wa BMT Allen Alex amesema ni vyema kuhakikisha vyama vinatekeleza majukumu yao kwa maendeleo ya michezo nchini.

kikubwa ni kuhakikisha viongozi wa kamati ya Paralimpiki Tanzania (TPC) wanakuwa karibu na vyama vyao wanavyovisimamia kufanya mashindano ili kupata wachezaji watakaoleta ushindani katika mashindano ya kimataifa, lakini pia kwa ajili ya kuwa hai basi walipe ada zao,”amesema Allen.

Kwa upande wake Makamu wa rais wa TPC Vincent Kaduma amewashukuru wadhamini waliojitokeza kusaidia kwa karibu watu wenye ulemavu na kufanikisha kufanyika kwa mashindano hayo wakiwemo kampuni ya Toyota, BMT pamoja na Gold Star.

“niwashukuru sana wadhamini wetu waliojitokeza kwa karibu kutushika mkono ili kufanikisha mashindano haya wakiwemo kampuni ya Toyota,BMT pamoja na Gold Star, mashindano haya hayajafanyika miaka kadhaa sasa ila kwa uwezo wa wadhamini wetu hawa tumeweza kufanikisha mashindano haya,”alisema Kaduma.