TENGA ASISITIZA VYAMA VYA MICHEZO KUWA NA MIPANGO KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO
service image
31 Jan, 2024

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Leodigar Chilla Tenga leo Januari 31, 2024 amekaa na wajumbe  wake wa Baraza la 15  katika kikao
kudadavua mambo mbalimbali kuendelea kuiweka michezo nchini sehemu nzuri kimaendeleo.

Aidha, Mwenyekiti alimtaka Katibu wake kutoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya kamati za michezo za mikoa pamoja na maendeleo ya utekelezaji wa Mfumo wa usajili kidigtali (SARS) kwakuwa ni sehemu ya maendeleo katika sekta hiyo.

Aliendelea kwa kuitaka sekretarieti kuvifuatilia vyama vya michezo vya taifa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa katiba zao, pamoja na kuvitaka kuwasilisha mipango ya maendeleo ya muda mfupi na muda mrefu ili kuendana na ushindani katika sekta ya michezo duniani

"Gharama za kuendesha michezo zinaongezeka na ushindani umekuwa Mkubwa, vyama vyetu lazima viwe na mipango kulingana na ushindani uliopo Duniani,"ilielezwa

Aidha, Mwenyekiti Tenga amesisitiza kuhusu kuweka mipango katika mambo mbalimbali sanjari na kuisimamia ili kufanikiwa katika kuendeleza sekta ya michezo nchini.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Baraza Bi. Neema Msitha amewaeleza  wajumbe juu ya utekelezaji wa mipango ya Baraza ambapo, baadhi ya Maafisa wapo Mikoani kuzitembelea kamati za michezo za Mikoa ili kuzikumbusha maeneo muhimu ya kutekeleza kwa mujibu wa Sheria na kanuni za Baraza na imepagwa kuzifikia kamati zote ili  kuendelea kupiga hatua ya maendeleo katika michezo.

Aliongeza kwa kusema kuwa, mfumo mpya wa usajili (SARS) umefanikiwa kwa kiasi kikubwa na elimu inaendelea kutolewa ili kuondoka katika mfumo wa kutumia karatasi, lakini pia, sekretarieti inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya michezo pamoja na maandalizi ya tuzo kwa wanamichezo Bora kwa mwaka 2024.