TLGU WEKEZENI KATIKA WACHEZAJI WA GOFU VIJANA ILI KUPATA WACHEZAJI WAPYA
Uongozi wa Chama cha Gofu wanawake (TLGU) umetakiwa kuwekeza zaidi katika wachezaji wa Gofu Vijana ili kupata wachezaji wapya watakaoleta chachu na ushindani zaidi katika mchezo huo pamoja na kupata wachezaji wazuri watakaounda timu ya Taifa.
Wito huo umetolewa leo tarehe 17 Septemba,2023 na Afisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Halima Bushiri wakati wa ufungaji wa mashindano ya Gofu wanawake 2023 yaliyofanyika katika viwanja vya Kiligolf Estate Mkoani Arusha.
“kwanza kabisa niwapongeze sana viongozi kwa kuandaa mashindano haya vizuri kabisa, lakini pia wadhamini mliojitokeza nawashukuru sana kwa kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuendeleza michezo yetu hapa nchini, viongozi niwaombe muendelee kuwekeza nguvu zaidi katika michezo ya vijana, ili tuweze kupata vipaji vipya vitakavyoleta ushindani zaidi katika mchezo huu pamoja na kupata wachezaji wazuri watakaounda timu ya Taifa,”amesema Halima.