TRU WATAKIWA KUPAMBANA NA USAJILI NGAZI ZOTE

Viongozi wa Umoja wa Mchezo wa Rugby Tanzania (TRU) wametakiwa kupambana na kukamilisha Katiba za ngazi zote kuanzia chini hadi Taifa ili wakamilishe usajili na hatimaye kuwa na wapiga kura kwa ajili ya Umoja wa mchezo huo ngazi ya Taifa (TRU).
Rai hiyo imetolewa leo tarehe 30 Septemba, 2022 na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Michezo Baraza la Michezo Halima Bushiri katika kikao na Uongozi wa TRU pamoja Viongozi wa Vilabu vya umoja huo kwa lengo la kujadili maendeleo ya mchezo huu nchini.
"Jitahidini kukamilisha katiba za baadhi ya vilabu ambavyo bado havijasajiliwa, wasilisheni kwa msajili ndani ya mwezi huu wa kumi ili usajili ukamilike na hatimaye uchaguzi wa TRU ufanyike,"alisema Halima.
Aidha, amewataka kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya umoja. huo pamoja na taarifa ya fedha.
Aliendelea kwa kuwataka Viongozi wa TRU kuwa wawazi, wawajibikaji, kusimamia nidhamu sambamba na ushirikishaji wa wadau weo katika yale wanayotekeleza ikiwemo mapato na matumizi.
Kwa upande wa Katibu wa TRU Jacob Dawa ameishukuru BMT kwa kukubali kikao nao na kusema kuwa watafuata maelekezo yote kuhakikisha wanapiga hatua zaidi.
Aidha, tarehe 01 Oktoba, 2022 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es salaam yatafanyika mashindano ya mchezo huo yatakayoshirikisha vilabu katoka katika mikoa zaidi ya kumi (10) nchini.