UNGUJA YAZIDI KUTAMBA WAVU NA KIKAPU UMITASHUMTA 2023
service image
07 Jun, 2023

Timu za Mpira wa Wavu na Kikapu Wavulana kutoka Kanda ya Unguja Visiwani Zanzibar, zimeendelea kutamba katika mshindano ya umoja wa Michezo na taaluma kwa wanafunzi wa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) yanayoendelea Mkoani Tabora.

Katika mchezo wa Mpira wa Wavu uliochezwa leo tarehe 7 Juni 2023 majira ya Saa 2 Asubuhi katika uwanja wa Shule ya Sekondari Wavulana Tabora, Timu ya Kanda ya Unguja iliibuka na ushindi baada ya kuifunga Timu ya Mkoa wa Simiyu kwa Seti 3-0.

Matokeo hayo yameifanya Unguja kuendelea kujiweka vizuri katika hatua zinazofuata, ikiwa hadi sasa imepoteza mchezo mmoja tu kati ya michezo mine ambayo imecheza katika michezo ya UMITASHUMTA mwaka huu.

Kwa upande wa mpira wa kikapu Wavulana, Timu ya Kanda ya Unguja imecheza michezo miwili leo tarehe 7 Juni 2023 katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Wavulana Tabora.

Mchezo wa kwanza ulianza Mjira ya Saa 2 Asubuhi na kumalizika kwa matokeo ya Ushindi kwa Unguja kushinda vikapu 25 dhidi ya Mwanza iliyopta vikapu 5, huku katika mchezo wa Pili uliochezwa Saa 5 Asubuhi Unguja ikiibuka na Ushindi mwingine wa Vikapu 34 dhidi ya Morogoro iliyoambulia Vikapu 2.

Matokeo haya yameifanya Timu ya Kanda ya Unguja kuwa Timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote kwenye kundi lake ikiwa inajiandaa na hatua inayofuata ya robo fainali.