ITUMIENI VIZURI MITANDAO YA KIJAMII KUISEMEA STARS
service image
30 Dec, 2023

Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imewataka Watanzania na wadau wa soka kutumia vizuri mitandao ya kijamii kusemea vizuri timu ya Taifa ya mpira wa miguu 'Taifa Stars' ili kuongeza hamasa kwa timu hiyo.

Rai hiyo imetolewa Disemba 30, 2023 na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa mkutano na waandishi wa habari kilicholenga kuongeza hamasa sambamba na kuisaidia Serikali kuzichangia timu za soka jinsia zote kuelekea katika michezo ya AFCON na WAFCON.

"Watanzania na wadau wa soka nchini tunatakiwa kubadilika kwa kusemea maneno mazuri Taifa Stars hasa kipindi hiki wanachoelekea kucheza michuano ya Africa (AFCON) nchini Ivory Coast," alisisitiza Waziri Ndumbaro.

Alisema watanzania wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kuipenda timu ya taifa pamoja na kutoa sapoti kwa lengo ya kuwapa hamasa wachezaji.

"Serikali itahakikisha inaendelea kuunga mkono timu ya taifa hasa kipindi hiki ambapo wapo kambini kujiandaa na michuano hiyo.

"Tunashukuru Serikali ya Zanzibar chini ya Rais wake, Hussein Ali Mwinyi kwa kuwapatia kambi ya siku tatu, wachezaji hao wa Taifa Stars wanaotarajia kuondoka kwenda Misri kati ya tarehe 30 Disemba, 2023 au tareh Mosi 2024, "alisema.

Dk. Ndumbaro aliongeza kuwa, Januari 10, mwaka huu wataendesha harambee ili fedha hizo zisadie timu zote mbili ya wanaume na wanawake kuelekea katika michuano hiyo ya Afcon na Wafcon.

Naye Naibu wa Wizara hiyo Hamisi Mwinjuma alisema Serikali ina mchango mkubwa katika kuhakikisha michezo inapiga hatua nchini.

"Tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha michezo inapiga hatua kwa sapoti yake, ikiwemo kuweka hamasa baada ya kuwepo ' Goli la Mama', "alisema.

Taifa Stars inatarajia kucheza michuano ya Afcon mwakani ambapo imepangwa kundi na timu za Morocco, Zambia na Jamhuri ya Kidemkrasi ya Congo 'DRC'.