VIJANA WATAKIWA KUWA WAZALENDO KWA TAIFA LAO

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila amewataka vijana nchini kuwa na mipango ya kujiendeleza kiuchumi na kijamii wakati bado wakiwa na nguvu, huku wakizingatia nidhamu na uzalendo kwa Taifa lao.
Chalamila ameyasema hayo tarehe 10 Oktoba,2022 wakati wa mdahalo wa vijana kuadhimisha wiki yao kitaifa uliofanyika mkoani Kagera.
"Zisakenu fursa muwezavyo wakati bado mkiwa vijana na wakati sahihi, kwani maisha yako ya mbeleni yanategemea na vile ambavyo umejiandaa tangu ukiwa kijana." amesema Chalamila
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa wa Kagera ametoa wito kwa vijana nchini kuendelea kuwa wazalendo na kutimiza majukumu yao mapema kabla muda haujapita, huku akiwataka viongozi kuwekeza kwa vijana.
Akizungumzia wiki ya vijana, Chalamila amewataka vijana kuyatumia maonesho hayo kuzungumza na Vijana wenzao wa Kagera na kutumia fursa mbalimbali zilizopo za uwekezaji na ujasiriamali .
Chalamila amewaomba wazazi na viongozi nchini kuendelea kuwapa fursa vijana pamoja na nafasi ya kuwasikiliza na kuwashirikisha kwenye maamuzi mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kuwa viongozi bora wa baadaye.