WACHEZAJI WA TIMU YA TAIFA YA KARATE WATAKIWA KUWEKA UZALENDO MBELE KATIKA MASHINDANO YA KIMATAIFA KWA NCHI ZA MAZIWA MAKUU
service image
13 Jul, 2023

Wachezaji wa Timu ya Taifa ya mchezo wa Karate Tanzania, wametakiwa kuwa wazalendo na kulipambania Taifa wanapokwenda kushindana katika mashindano ya kimataifa kwa nchi za Maziwa Makuu yanayotarajiwa kuanza tarehe 18 Julai, 2023 nchini Congo.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 13 Julai, 2023 na Afisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Nicholaus Mihayo, alipotembelea kambi ya timu hiyo iliyopo Lamada Hotel- Ilala Jijini Dar es Salaam, kushuhudia maandalizi ya timu pamoja na kutoa hamasa kwa wachezaji, ambapo amewasihii kuendelea kujituma mazoezini kwani serikali na Taifa linawategemea kufanya vizuri katika mashindano hayo ya kimataifa.

“kikubwa hasa ninachotaka kuwaambia ni nyinyi kuweka uzalendo mbele mnapokwenda katika mashindano haya makubwa, mkalipambanie Taifa pamoja na kutunza nidhamu nafahamu kuwa kuna baadhi yenu wachezaji mmetoka katika vyombo vya ulinzi na usalama, ni vyema maana tunajuwa nyinyi ni wazalendo mtakwenda kuliheshimisha Taifa na kufanya vizuri katika mashindano haya,”amesema Mihayo.